Pekua michezo hapa
Simba, Yanga zafukuza makocha tisa miaka mitatu
Dar es Salaam. Wakati
Yanga imesitisha mkataba wa kazi wa kocha wake, Ernest Brandts
imebainika kuwa Yanga na Simba zimefukuza makocha tisa kwa kipindi cha
miaka mitatu.
Simba ndiyo inayoongoza kwa kuwatimua makocha watano wakati Yanga imefungisha virago makocha wanne kuanzia 2010 hadi 2013.
Makocha waliokumbwa na mkasa wa kutimuliwa kwa
upande wa Simba ni Patrick Phiri (Zambia), Milovan Cirkovic (Serbia),
Moses Basena (Uganda), Patrick Liewig (Ufaransa) na Mtanzania pekee
Abdallah Kibadeni.
Yanga iliwatimua Sam Timbe (Uganda), Kostadin Papic (Serbia), Tom Saint Fiet (Ubelgiji) na Ernest Brandts kutoka Uholanzi.
Kwa kuanzia na Phiri (56) aliteuliwa kuifundisha
Simba Septemba 9,2009 na akatimuliwa Aprili 19, 2011 huku akiwa
amefanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu mara mbili 2004-5 na 2009-10,
Kombe la Tusker 2005 na Kombe la Kagame 2006.
Baada ya Phiri kuondolewa, Simba ilimtwaa Basena
ambaye alidumu kwa muda wa miezi sita pekee baada ya kusitishiwa mkataba
Novemba mwaka huohuo na nafasi yake kuchukuliwa na Milovan
aliyeiwezesha Simba kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu na kuifikisha timu hiyo
katika hatua ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Licha ya kuifikisha Simba katika hatua ya 16 bora
ilipofika Oktoba 2012 Milovan aliondolewa na nafasi yake ilichukuliwa na
Liewig ambaye naye alilazimishwa kukusanya kila kilicho chake Juni
mwaka huu na kumkabidhi majukumu Kibadeni aliyefurushwa mara tu baada ya
mzunguko wa kwanza kukamilika Novemba mwaka huu.
Katika kipindi hicho, Yanga ilikuwa hivi, Timbe
aliyeiwezesha Yanga kutwaa ubingwa wa ligi na Kombe la Kagame
alitimuliwa Novemba 2012 na nafasi yake ikachukuliwa na Papic ambaye Mei
mwaka jana mkataba wake ulisitishwa na nafasi yake ikachukuliwa na
Saintfiet ambaye alipigwa chini miezi mitatu baadaye na timu kukabidhiwa
kwa Brandts aliyesitishiwa mkataba siku chache zilizopita.
Hivi sasa Simba iko chini ya Kocha mpya, Zdvacko
Logarusic kutoka Croatia na Yanga iko katika mchakato wa kutafuta kocha
mpya huku ikimwondoa kocha msaidizi, Fred Felix Minziro na nafasi yake
inatarajiwa kuchukuliwa na Boniface Mkwasa.

No comments:
Post a Comment